ULEGA AWATAKA WAFUGAJI PWANI KUVUNA MIFUGO YAO

Imewekwa: 30, September 2021

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amewataka Wafugaji wa Mkoa wa Pwani kuanza kuvuna Mifugo yao na kuiuza kwani kwa kufanya hivyo kutawasaidia kuwaongezea kipato na kupunguza migogoro kati yao na watumiaji wengine wa ardhi.

Ulega aliyasema hayo Septemba 19, 2021 wakati akiongea na Wafugaji na Wakulima wa Wilaya ya Rufiji alipofanya ziara Wilayani humo ya kusikiliza kero zao na kuzitafutia ufumbuzi.

Alisema ni muhimu viongozi wa Wilaya za Rufiji, Mkuranga na Kibiti kukaa na wadau wa mifugo kutengeneza mkakati wa kuhamasisha uvunaji wa mifugo yao kwakuwa soko la kuuza lipo mkoani humo na bado hawajalitumia ipasavyo.

"Hapa Mkoa wa Pwani tuna Kiwanda cha Nyama cha TanChoice lakini pamoja na kiwanda hicho kuwepo hakuna mifugo inayopelekwa pale kutoka ukanda wetu huu wa Pwani," alisema Ulega

Aliongeza kwa kusema kuwa ili faida ya uwepo wa kiwanda hicho ionekane ni vyema wadau wote wa mifugo mkoani humo waanze uvunaji mkubwa na kupeleka kuiuza kiwandani hapo.

"Tunatamani kuona mifugo inatoka katika ukanda huu wa Pwani na kwenda kuuzwa jijini Dar es Salaam ambapo ndipo kwenye biashara kubwa ya nyama, msione fahari kukaa na makundi makubwa ya mifugo ambayo mwisho wa siku yakaonekana kuwa ni kero na hayana faida," aliongeza Ulega

Kuhusu kuboresha huduma za Mifugo, Waziri Ulega alisema kuwa katika Bajeti ya Mwaka huu 2021/ 2022 Serikali ya Awamu ya Sita ya Rais Samia Suluhu Hassan imepanga kununua Pikipiki 300 na itazigawa kwa Maafisa Ugani nchi nzima ili waweze kutoa huduma ya mifugo kwa ufanisi.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Meja Edward Gowelle alisema kuwa kufuatia migogoro mingi iliyoibuka katika Wilaya yake ameanzisha zoezi la sensa ya Mifugo na Wafugaji ili waweze kujua idadi yao halisi na kupanga mipango ya matumizi bora ya ardhi kulingana na mahitaji.